ADVERT

13 January, 2011

Jeshi kizio cha uuaji wa demokrasia

Tusiandike tukiogopa jeshi?tusiseme tukiogopa jeshi?tusitende tukiogopa jeshi? Jeshi ni nini haswa? Jeshi latoka wapi haswa? Kwanini linakuwa na nguvu na ubabe ambao hawana? Kwanini jeshi linadumaza jitihada za kukuza demokrasia?

Natambua jeshi lina jukumu kubwa la kulinda mali za raia na raia wenyewe. Jeshi lina jukumu la kuhakikisha usalama katika nchi. Lakini jeshi halina mamlaka ya kufisha demokrasia. Jeshi halina mamlaka ya kufisha uhuru wa watu kujieleza!

Mmoja ya raia akidhibitiwa asiandamane na Jeshi la Polisi

Ni mara ngapi jeshi limefisha uhuru wa raia pasi kujulikana? Ni mara ngapi jeshi limefisha uhuru wa raia na ikajulikana hadharani? Ni mara ngapi jeshi limetumia ubabe pasi umma mzima wa watanzania kufahamu? Watu wenye kuguswa na utendaji wa jeshi la Tanzania wanayo mengi ya kueleza. Wafungwa na mahabusu magerezani wanamengi ya kueleza juu ya utendaji wa jeshi la Tanzania. Si mnaukumbuka ule usemi; “wanaokwenda jela siyo wote wana hatia?”

Ni mara ngapi baadhi ya jumuiya za kiraia zinapenda kufanya matukio ya kidemokrasia ambayo kwa namna moja yanachangia katika ukuaji na uboreshwaji wa demokrasia yetu wanakumbana na vigingi vya utendaji kwa kile kinachoitwa “taarifa za kiintelijensia”?

Kama nguvu kubwa inaweza kutumiwa kwa taasisi kubwa za kidemokrasia nchini kama vyama vya kisiasa tena vyama vikubwa vya kiupinzani hali itakuwaje kwa asasi za kiraia? Hali itakuwaje kwa mwananchi mmoja mmoja?

Ama tumeshahau yaliyotokea Januari, 2001 kule Zanzibari kwa wananchi waliotumia haki ya kibinadamu ya kujieleza kwa aina ya maandamano? Je yaliyotokea yanautofauti na ya Januari, 2011 kule Arusha?

Asasi moja ya kiraia tena ya vijana waliokuwa na utashi wa kuhamasisha wananchi hususan vijana wenzao kujitokeza kupiga kura kwani waliona historia inaonyesha ushiriki mdogo wa vijana katika michakato ya uchaguzi. Wakatumia rasilimali muda na fedha achilia mbali ari na utashi waliowekeza lakini wakaambulia siku moja kabla ya tukio kuzuiliwa kufanya tukio baada ya kutengua kibali ambacho walikiidhinisha wenyewe polisi ati nini, “taarifa za kiintelijensia”!

Hatukusikia kilio chao na namna walivyofafanua tukio zima la utumiaji wa mabavu ya kiutendaji jeshi hilo kuondosha utashi wa kukuza demokrasia?

Ni rahisi sana kwa jeshi hili kuandika barua na kuitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza kile wakiitacho “taarifa za kiintelijensia” kusitisha tukio lililoandaliwa kwa muda mwingi pasi kulipa fidia. Ndiyo, kwanini wasiwe wanalipa fidia hasa kwa utenguaji wa vibali ambavyo wanakuwa wamekwisha vitoa?

Kama ilivyojidhihirisha kwa jeshi la polisi kuwa na uwezo wa kutumia nguvu ya ziada hata ambako hakuna hitaji hilo katika kupambana na kuzuia maandamano, wakati wangeweza kwa nguvu nusu ama ndogo zaidi ya nusu itumikayo kudhibiti maandamano kuitumia kuhakikisha usalama “crowd control” kama ambavyo wanatarajiwa wafanye. Lakini loh salale!



Nikijali afya ya nchi kidemokrasia kwa kuhakikisha vyombo vya dola vinakuwa sehemu ya kukuza demokrasia natarajia kuwaona wakiguswa na madoa ya damu ambazo wanamwaga zisizo na hatia. Uhai uliokatishwa utaendelea kuishi daima na kuwabughudhi hata katika njozi na endapo kutakuwa na ulegevu kalamu, hotuba na machozi ya wafiwa yataendelea kububujika na kuandika historia kizazi hata kizazi zikililia damu azizi iliyomwagwa.

Polisi wasisahau wanaowapoteza maisha ni kaka na dada zetu, ni baba na mama zetu, zaidi ni sehemu ya jamii yetu. Wanapaswa watambue kila hatua wanayoitenda ina athari katika jamii ambayo wao na vizazi vyao vinaishi.

Wasisahau risasi, bunduki, mavazi hata mishahara inayowapa nguvu kuamrisha watu kumwaga damu, na wale wapokea amri kutii na kutekeleza ni kutokana na kodi za wananchi hao hao wanaowaua na kumwaga damu. Hii akili kweli?

Tayari wananchi wameanza kuwa na ujasiri wa kujiuliza kama alivyoainisha Padri Privatus Karugendo; “Kwani Tanzania tuna risasi ngapi? Tunazo milioni 40? Tuna polisi wangapi? Tunao milioni 40? Watanzania sasa hivi wanakimbilia milioni 40, wakishikamana hakula la kuwafanya”! Hakika Jeshi la Polisi likiendelea kutenda litendayo litawafanya wananchi nchi nzima kutenda chochote, haya ndiyo matunda ya kujificha nyuma ya “taarifa za kiintelijensia”.

Waogope nini kama ameshuhudia askari ambaye alitegemea amlinde akimpiga risasi kaka yake? Unategemea atende nini endapo alishuhudia askari akimpiga mama mjamzito mbele ya macho yake? Unataka atende nini endapo aliona askari akitoa uhai wa baba yake aliyemtegemea kimaisha? Hiki ndicho kizazi kinachozalishwa kwa kazi ya polisi ya “taarifa za kiintelijensia”.


Mmoja wa wahanga wa nguvu ya Polisi katika maandamano umauti ukiwa umemkuta baada ya kupigwa na risasi


Tanzania imeshabarikiwa amani na utulivu, Watanzania wameshabarikiwa tunu za kutunza amani na utulivu katika mioyo yao. Watanzania mmoja mmoja ama hata katika jumuiya za kiraia kama asasi za kisiasa na za kiraia hawana jeshi wala si wengi wenye bunduki kulinganisha bunduki zilizopo katika majeshi ya usalama. Usalama wao na matumaini yao ya amani yamewekezwa kwenye majeshi ya usalama kama jeshi la polisi na kudiriki kuligharamia kwa kodi zao.

Jeshi likitaka lilinde amani kama tunavyotarajia wao kutimiza jukumu lao hilo katika jamii yetu lakini pia likitaka linaweza likaendelea kupuuza na kuenenda na vitendo vyake vya kuondosha amani na utulivu!

Mfungwa Mswahili alishasema katika hotuba yake;“Ndugu waheshimiwa jiheshimuni, waheshimuni na wengine mpate kuheshimika kihalali, jiheshimuni ndipo mdai heshima”.

© Michael Dalali, 2011

No comments: